Kilio cha Wakimbizi wa Burundi

Siku ya kimataifa ya wakimbizi duniani iliadhimishwa Jumatatu, ikiwa ni siku ya kuwakumbuka na kuwatambua zaidi ya watu milioni nne waliotapakaa sehemu mbali mbali duniani baada ya kupoteza makazi.

Image caption Mmmoja wa wakimbizi kutoka Burundi

Wakati wakimbizi kutoka nchi mbali mbali walioko katika Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo wakikusanyika mjini Kinshasa kupata mafunzo kuhusu haki zao, ilikuwa ni majonzi kwa wakimbizi kutoka Burundi ambao wamekuwa wakiishi Tanzania.

Kwenye kambi ya wakimbizi ya Mutabila iliyoko wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, siku hiyo iliadhimishwa kwa ilani kutolewa kwa zaidi ya wakimbizi elfu 35 kutoka Burundi walioko katika kambi hiyo, kuwa lazima warejee nyumbani.

Hakuna usalama

Serikali ya Tanzania inataka kambi hiyo kufungwa ifikapo tarehe 31 Disemba mwaka huu, na kwa hivyo wakimbizi wametakiwa kuanza kujiandaa kurudishwa nyumbani kuanzia mwezi Septemba.

Lakini wakimbizi hao baadhi yao walioishi Tanzania kwa karibu miaka 40 wanapinga pendekezo la kuwarudisha nyumbani Burundi, wakisema usalama uliopo hauridhishi.

'' Hali iliyo dhahiri ni kuwa vyombo vya habari nchini kwetu vinatangaza kuwa hakuna usalama wa kutosha. Taarifa hizo hutufanya wakimbizi tuogope sana maana aliuwawa mwenzetu, na aliyeumwa na Nyoka akiona unyasi hushtuka.'' Alisema msemaji wa wakimbizi hao.

Kambi ya Mutabila ni ya mwisho kwa wakimbizi kutoka Burundi ambao wamekuwa wakiishi Tanzania, baada ya kambi zingine mkoani Kigoma kufungwa.

Wengi wa wakimbizi waliokimbia Burundi kutokana na machafuko ya mwaka wa 1972 wameshapata uraia wa Tanzania , lakini wale ambao hawakuweza kupata uraia, pamoja na wakimbizi wengine walioingia nchini humo baada ya vita mwaka 1993 walipelekwa katika kambi ya Mutabila kusubiri kurejeshwa nyumbani.

Image caption Kambi ya Mtabila

Mwakilishi wa serikali ya Tanzania Idd Mpoma alisema wakati huu lazima wakimbizi waondoke kuanzia Septemba.

'' Hilo halibadiliki, kwa hivyo ni wakati wa familia kukaa kufikiria swala la kurejea, kinyume na hapo mtapata taabu nyie.''

Kwaya ya wakimbizi hao ilitunga wimbo maalumu kuwataka viongozi wa Tanzania kuwaongeza muda na kuelewa kuwa hawakujiombea kuwa wakimbizi.

Warejee kwao

Jumla ya wakimbizi zaidi ya 600,000 kutoka Burundi waliomba tokea mwaka wa 1972.

Warundi laki moja na elfu sitini wa kambi ya Katumba na Mishamo mkoa wa Rukwa mwaka jana walipewa uraia wa Tanzania.

Lakini wakimbizi 35,000 waliosalia wanatakiwa warejee kwao Burundi.

Mvutano uliojitokeza baina ya wakimbizi ,serikali za Burundi na Tanzania pamoja na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR umeacha swala hili kwenye njia panda, kuhusu nini kitatokea kuanzia mwezi Septemba wakati kundi la kwanza la wakimbizi elfu kumi litatakiwa kusafirishwa hadi Burundi.