Nato yapoteza ndege yake Libya

Msemaji wa majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya, Nato amesema helikopta moja isiyotumia rubani imepotea huko Libya.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Libya

Kamanda Mike Bracken alisema kituo cha Nato huko Naples kilipoteza mawasiliano na ndege hiyo majira ya asubuhi.

Alisema, helikopta hiyo ilikuwa ikiipeleleza Libya " kuchunguza majeshi ya kiongozi Muammar Gaddafi yanayotishia raia."

Kamanda Bracken alisema hakuna helikopta zozote za mashambulio zilizopotea.

Alisema, "Tunajitahidi kutafuta sababu za kupotea kwa helikopta hiyo."

Awali, televisheni ya taifa ya Libya ilisema majeshi ya serikali yalilipua helikopta ya Apache kwenye wilaya ya Zlitan magharibi mwa nchi hiyo.

Nato ilisambaza helikopta za mashambulizi za Apache za Uingereza na Ufaransa nchini Libya mapema mwezi huu wakati wa ujumbe wake uliodhaminiwa na Umoja wa Mataifa wa kulinda raia kutoka kwa majeshi yanayomtii Kanali Gaddafi.