Siendi popote- Gyan

Gyan
Image caption Asamoah Gyan

Mshambuliaji wa Sunderland Asamoah Gyan ametupilia mbali taarifa zinazosema anahama, akisema hana mpango wa kuondoka.

"Siondoki Sunderland, sibabaishwi na uvumi uliozagaa katika magazeti na tovuti," amesema Gyan akizungumza na tovuti ya MTNFootball.com.

Gyan kutoka Ghana, alifunga magoli 11 katika msimu wake wa kwanza katika ligi ya England.

"Nimejitolea kuichezea Sunderland kwa sababu napenda klabu na utamaduni wake," amesema Gyan.

"Nitabakia Sunderland msimu ujao, na katika siku zijazo, na nasubiri kwa hamu kukutana na wachezaji wenzangu na mashabiki wa Sunderland, tutakaporejea mwezi ujao."

Gyan ni mchezaji wa bei ghali zaidi kununuliwa na Sunderland, akitokea klabu ya Rennes ya Ufaransa kwa kitita cha zaidi ya pauni milioni 13, mwezi Agosti mwaka 2010.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Sunderland, kutokana na mtindo wake na ufungaji wa magoli muhimu, likiwemo goli la kusawazisha katika dakika za majeruhi dhidi ya Newcastle mwezi Januari 2011.