Raia wa Ethiopia walioko Yemen kuondolewa

Wakimbizi wakishauriana na maafisa wa Umoja wa Mataifa Haki miliki ya picha AP
Image caption Wakimbizi wakishauriana na afisa wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteres na mjumbe wake maalum Angelina Jolie.

Takriban raia 2,000 wa Ethiopia ambao wamekwama nchini Yemen, inayokumbwa na mzozo wa kisiasa wataondolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika masuala ya uhamiaji, IOM.

Shirika hilo limesema tayari limewahamisha raia 275 wa Ethiopia, baadhi yao wakiwa na majeraha ya risasi.

Kwa kipindi cha miezi kadhaa sasa Yemen, imekumbwa na ghasia zinazotokana na rais wa nchi hiyo kukataa kuondoka mamlakani, jambo ambalo upinzani unashinikiza lifanyike.

Raia wawili wa Somalia walifariki dunia mwezi uliopita katika mji mkuu wa Sanaa.

Yemen imekuwa ikitumika kama njia ya wahamiaji haramu kutoka upembe wa Afrika wanaoelekea barani Ulaya.

Shirika la IOM limesema walanguzi wa watu wanatumia kipindi hiki cha machafuko nchini Yemen kupeleka watu zaidi kutoka Ethiopia na Somalia.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linakadiria kuwa watu 37,000 kutoka Ethiopia na Somalia wamepelekwa nchini Yemen mwaka huu.

Watu hao walitarajia kuwa watasafiri hadi Saudia Arabia lakini wengi wamekwama kwenye kambi karibu sana na mpaka wa nchi hiyo na Saudi Arabia.