Gaddafi ashtumu Nato kwa mauaji

Kiongozi wa Libya Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kiongozi wa Libya Kanali Muamar Gadaffi.

Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi ameshtumu mataifa yanayounda muungano wa Nato kwa mauaji,siku mbili baada ya watu wa familia ya mshirika wake wa karibu kuuawa kufuatia shambulio la angani.

Kupitia kituo cha taifa cha Televisheni,alitoa ujumbe kwa kanda siku ya Jumatano, akielezea wale waliotekeleza mashambulio kama "wahalifu" na "makatili".

Nato imeomba radhi kwa vifo vya raia, lakini wakasema kuwa nyumba iliolengwa ni "kituo kinachoratibu harakati za vikosi vya Gaddafi".

Jamii ya kimataifa imegawanyika

Mapema waziri wa mambo ya nje wa Italia alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja.

Francisco Frattini alisema muhimu mapigano yasitishwe ili kutoa fursa kwa misaada kuwafikia raia.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Jengo la serikali ya Libya lililoharibiwa kufuatia shambulio la bomu lililotekelezwa na NATO

Pia akataka Nato kutoa taarifa zaidi kwa harakati zake za mashambulio ya angani na utaratibu mahsusi wa "makosa yaliyowalenga raia".

Lakini katibu mkuu wa Nato, Anders Fogh Rasmussen,alisema mashambulio ya angani ni ya kuwalinda raia na yataendelea.

Alisisitiza kuwa Nato inachunguza taarifa za Libya kwamba watu saba wameuawa kutokana na mashambulio ya angani wiki iliopita, lakini akasema kuwa ni vikosi vya Kanali Gaddafi vinavyolenga raia, wala sio Nato.