Mashambulizi yakomeshwe Libya

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Italy Franco Frattini ametoa wito wa kusimamishwa mashambulizi nchini Libya ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kupelekwa nchini humo.

Image caption Franco Frattini waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Italy

Bw.Frattini pia amesema Nato inapaswa itoe maelezo kwa kirefu kuhusu matokeo ya kampeini yake dhidi ya vikosi vya serikali ya Libya na vile vile kuhusu muongozo ikiwa makosa yatafanywa wakati wa kulenga shabaha.

Mwenyekiti wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu Amr Moussa pia nae ametoa wito wa kusitishwa mapigano akizungumzia kutoridhishwa na namna kampeini ya kikosi cha Nato inavyoendeshwa hivi sasa.

Siku ya Jumapili kombora la Nato lilishambulia makazi ya watu kwa makosa. Serikali ya Libya imesema watu tisa ikiwa ni pamoja na watoto wawili waliuawa katika shambulizi hilo.

Kikosi cha Nato kwa upande wake kina kiri kuwa huenda raia wasio na hatia walijeruhiwa katika tukio hilo.

Wakati huohuo waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uchina Yang Jiechi amesema kundi la waasi linalojiita "baraza la upinzani la kitaifa kuhusu mabadiliko nchini Libya" ni mwenza muhimu katika mazungumzo ya upatanishi na vile vile ni kundi madhubuti la siasa za nyumbani.

Kiongozi wa waasi hao Mahmoud Jibril amekuwa akifanya mazungumzo na uwongozi wa Uchina mjini Beijing.

Akizungumza katika bunge la waakilishi la Italy Bw.Frattini ametoa wito wa kusimamishwa mashambulizi kutoa fursa ya misaada inayohitajika sana kuingizwa nchini humo.

Kuhusu shirika la kujihami la Nato, amesema ni muhimu kutoa maelezo yaliokamilika ya matokeo ya kampeini yake na vile vile kufafanua kuhusu muongozo uliopo ikiwa makosa yatafanywa na kuwadhuru raia wakati wa kampeini yake dhidi ya vikosi vya Libya.

Lakini wizara ya Mashauri ya kigeni ya Ufaransa inapinga kusitishwa kwa mashambulizi ikisema kuwa hatua kama hiyo itampa kanali Muammar Gaddafi muda wa kujiandaa kwa makabiliano zaidi.

Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika Jean Ping amesema anaamini mataifa ya magharibi hatimae yataukubali mpango wa Muungano wa Afrika wa kukomesha mashambulizi na kufungua njia ya kufanya mabadiliko muhimu yanayohitajika.

Jean Ping hakuzungumzia suala la kufurushwa kanali Gaddafi, suala ambalo upinzani unapania sana na kulipa kipaumbele katika masharti yake ya kuleta maelewano Libya.