Wanajeshi 33,000 kuondoka Afghanistan

Rais Obama
Image caption Rais wa Marekani Obama

Rais Barack Obama ametangaza kuondoa wanajeshi 10,000 wa Marekani kutoka Afghanistan mwaka huu na wengine 23,000 kufikia mwezi Septemba mwaka 2012.

Akizungumza kutoka ikulu ya rais wa Marekani ya White House, amesema "huu ni mwanzo,lakini siyo mwisho wa juhudi zetu za kumaliza vita hivi".

Idadi hii ya wanajeshi ni kubwa na tena wanaondolewa kwa haraka zaidi,kinyume na ushauri uliotolewa na makamanda wa kijeshi.

Makamanda walikuwa wamemwambia rais kwamba mafanikio yaliopatikana ya kuimarisha usalama yangetiwa doa na hata hali kurudi kama ilivyokuwa,na kutoa pendekezo la kuwa na idadi kubwa ya wanajeshi hadi mwaka 2013.

Hata hivyo, takriban wanajeshi 68,000 wa Marekani watabaki nchini Afghanistan. Wanajeshi wote ambao wako kwenye mapigano wataondoka kufikia mwaka 2013, na wakati huo inatarajiwa maafisa wa usalama wa Afghanistan wataweza kusimamia majukumu ya usalama wao wenyewe.