Rais Bashir kufunga mabomba ya mafuta

Rais Omar al-Bashir wa Sudan ametishia kufunga mabomba yanayosafirisha mafuta kutoka Kusini mwa Sudan ikiwa mpango muafaka kuhusu suala la mafuta hutoafikiwa kabla Sudan Kusini kuanza kujitawala mwezi Julai.

Image caption Rais Bashir wa Sudan

Amesema Sudan Kusini inaweza kuendelea kutoa nusu ya pato lake la mafuta kwa Sudan Kaskazini ama ilipie kutumia miundombinu ya Kaskazini katika utaratibu wa kusafirisha mafuta.

Bw. Bashir amesema ikiwa hakuna litakalozingatiwa kati ya hayo mawili basi atafunga mabomba yote ya mafuta.

Theluthi tatu ya mafuta ya Sudan yako Sudan Kusini lakini mabomba mengi, viwanda vya kusafishia mafuta na bandari kuu vyote viko Sudan Kaskazini.

Sudan Kusini ilipiga kura ya maoni mwezi January kutaka kujitawala.

Rais Bashir alitoa vitisho hivi katika hotuba yake aliyoitoa mjini Port Sudan kuliko bandari kuu inayotumika kusafirisha mafuta.Hotuba yake hiyo ilionekana katika televisheni ya taifa.

Mazungumzo bado yanaendelea kati ya Kaskazini na Kusini mwa Sudan kuhusu mafuta na masuala mengine nyeti kabla ya Sudan Kusini kujitawala, ikiwa ni pamoja na suala la uraia na lile la eneo linalozozaniwa la Abyei.

Mwezi jana, jeshi la Sudan Kaskazini lilikamata eneo la Abyei lakini kumekuwa na makubaliano yalioafikiwa Jumatatu ambayo yanatoa fursa ya kuondolewa wanajeshi hao kutoka eneo hilo na kupelekwa wanajeshi wa Ethiopia katika eneo hilo kudumisha amani.