Swaziland yaomba fedha Afrika Kusini

Image caption Mfalme Mswati wa Swaziland

Afisa mwandamizi wa masuala ya mambo ya nje wa Afrika Kusini alisema, Swaziland imeiomba Afrika Kusini kuiokoa kutokana na kuelemewa na madeni kwani iko hatarini kufilisika.

Afisa huyo, Jerry Matjila, aliwaambia wabunge mjini Cape Town kwamba Swaziland ilihitaji pesa hizo kulipa wafanyakazi wa serikali.

Upinzani wa Afrika kusini umesema ombi hilo linatakiwa kukataliwa kwasababu Swaziland lilikuwa " taifa lisilofuata demokrasia".

Swaziland ni moja ya nchi maskini za Afrika na inaongozwa chini ya utawala wa kifalme moja kwa moja

Bw Matjila, anayeongoza idara ya uhusiano wa kimataifa ya Afrika Kusini, alisema Pretoria wamekuwa wakijadili ombi hilo.

Shirika la habari la Bloomberg limemnukuu Bw Matjila akisema, " Swali ni kwamba tunaweza kusaidia kwa kiwango gani. Tunataka bara lenye utulivu. Tunaanza na majirani zetu".