BBC Yataka mwandishi wake aachiliwe huru

Waandishi wa habari wa BBC wanafanya mkusanyiko maalum jijini London kumkumbuka na kudai kuachiliwa huru kwa mfanyakazi mwenzao anayezuiliwa nchini Tajikistan.

Image caption Urunboy Usmonov

Urunboy Usmonov amezuiliwa kwa kipindi cha siku kumi katika kituo kimoja cha idara ya usalama wa taifa katika eneo la Khojand, Tajikistan kaskazini.

Mapema wiki hii alishtakiwa rasmi kwa kuhusika na kundi lenye kufuata siasa za msimamo mkali. BBC imesema madai kuwa Bw Usmonov ni mfuasi wa kikundi cha Kiislamu kilichopigwa marufuku Hizb ut-Tahrir hayana msingi hata kidogo.

Hali

Baada ya kuzuiliwa kwa zaidi ya wiki nzima bila ya mawasiliano yoyote, familia yake sasa imeruhusiwa kumuona kwa kipindi cha nusu saa.

Mkewe Bw Usmonov, Malohat Abduazimova, ameiambia BBC jinsi walivyoshtushwa na hali ya mume wake.

"Sikuweza hata kumtambua", alisema. "alikua myonge na amekonda sana. Hata hakuweza kutembea. Niliona jinsi alivyopata shida kumpa mkono kaka yake. Siwezi hata kueleza."

Familia yake imekua na wasiwasi kuhusu Bw Usmonov ambae anaugua kisukari na matatizo ya moyo.

Alipokua korokoroni idara ya usalama iliwaruhusu waandishi habari wawili kumhoji Bw Usmonov. Katika ripoti yao waandishi hao walikariri tuhuma zinazomhusisha Bw Usmonov na kundi la Hizb ut-Tahrir .

Shirika la BBC lilitoa taarifa ikilaani makala hayo kuwa yalikiuka utaratibu wa kisheria na ukiukwaji mkubwa wa dhana ya mtuhumiwa kuzingatiwa hana hatia mpaka mahakama ikute vinginevyo.

Image caption Usmanov

Ilitetea haki ya waandishi wa BBC kuwahoji watu wa maoni tofauti na pia kuficha vyanzo vya ripoti zake zote.

Bw Usmonov amesema alikutana na wafuasi wa Hizb ut-Tahrir kama sehemu ya kazi yake ya uandishi, akiripoti kuhusu kikundi ambacho kinaendesha harakati zake katika eneo zima la Asia ya kati.

Alipigwa

Mahirika yanayotetea uhuru wa vyombo vya habari yamelaani kukamatwa kwake kama ni njama za kubana waandishi wasiripoti masuala nyeti ya kidini na kisiasa.

Bw Usmonov alikamatwa kwanza Jumaatatu Juni 13. Nyumba yake ilipekuliwa na familia yake wanasema waliona majeraha usoni mwake - ishara kuwa alipigwa.

Kumekuwepo na madai kadhaa kutoka kwa serikali za Uingereza, Marekani na Muungano wa Ulaya kutoa ufafanuzi kuhusu kesi hii.

BBC inaendelea kudai Bw Usmonov aachiliwe mara moja.

Image caption Usmanov akiwa kazini

Mwenzake mmoja aliyefanya nae kazi alimsifu kwa kazi yake na ubinaadamu wake

"Ni ushujaa na ukarimu wake ndio sifa zake. Ni mojawapo wa mtu adimu ambae uadilifu kwake ni kitu cha kawaida. Katika nchi ambayo imegawanyika vibaya kisiasa. Urunboy ni mtu wa msimamo wake mwenyewe. Yeye hachagui kundi lipi zuri ama lipi baya, bali tu hali ya maisha ilivyo".