Masoko ya Mihadarati yaanguka

Dawa aina ya Cocaine
Image caption Masoko ya Mihadarati yanaanguka

Shirika la umoja wa mataifa linalohusika na dawa za kulevya na uhalifu UNODC, linasema kuwa masoko ya dunia kwa mihadarati kama Cocaine, Opium na bangi yanaendelea kuanguka.

Lakini katika ripoti yake ya kila mwaka shirika la UNODC limesema uzalishaji wa madawa yasio asilia kunazidi kuongezeka.

Ripoti hiyo kuhusu matumizi ya dawa za kulevya duniani inasema ukulima wa kasumba katika Afghanistan,ambako hukuzwa asilimia 74 ya kasumba duniani kulipungua kwa kiwango cha asilimia 38 mwaka jana , kwa sababu ya maradhi yaliyoangamiza sehemu kubwa ya zao la maua yanayozalisha kasumba.

Lakini shirika hilo la umoja wa mataifa la kupambana na uhalifu na dawa za kulevya UNODC limeonya kwamba haielekei kwa hali hii ya kupungua uzalishaji kasumba utaendelea.

Ripoti inasema ulimaji wa zao la opium katika Burma uliongezeka kwa asilimia 20 mwaka jana.

Na ilionya kuwa kusini Mashariki mwa Asia imegeuka kuwa kituo kikuu kwa sababu ya kuongezeka sana kwa dawa zisizo asilia.

Ilisema matumizi mabaya ya dawa za matibabu ni tatizo linalozidi kukua.

Ripoti hiyo inasema utengenezaji wa Cocaine ulipungua lakini bado kuna matumizi makubwa ya mhadarati huo katika Marekani na Ulaya.