Rwanda yachapwa na Uruguay

Goli katika dakika za majeruhi kutoka Uruguay, lilizima matumaini ya Rwanda kupata pointi yake ya kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.

Image caption Rwanda U 17

Licha ya kupoteza mchezo huo, Rwanda bado kimahesabu ina nafasi ya kusonga mbele na kuingia katika timu 16, iwapo itashinda mchezo wake wa mwisho katika kundi c watakapocheza na Canada, juni 25.

Goli hilo pekee kwenye mchezo uliochezwa nchini Mexico lilipatikana katika dakika tano za nyongeza, baada ya kipa wa Uruguay kupiga mkwaju wa adhabu uliomkuta Leonardo Paris aliyefunga kwa kichwa.

Rwanda ilianza mchezo huo vizuri, na ilimiliki mpira mapema, na hata kupata nafasi za karibu kufunga magoli, kutokana na mipira miwili ya adhabu iliyopigwa na nahodha Emery Bayisenge.

Mkwaju wa kwanza uligonga mwamba, la wa pili ukipita juu kidogo ya mwamba.

Mtiririko wa timu ya Rwanda maarufu kama Dondola watoto, uliharibika baada ya meneja Richard Tardy kulazimika kufanya mabadiliko, kutokana na jeraha la goti la beki Faustin Usengimana.

Uruguay ilinufaika na mabadiliko hayo, na kuaza kufanya mashambulizi.

Rwanda ilifanikiwa kupiga mikwaju miwili katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda yoyote.

Uruguay ilimiliki kipindi cha pili.

Ushindi huu unamaanisha Uruguay wanasonga mbele katika timu 16, na watapambana na England Juni 25. England walitoka sare ya 2-2 na Canada katika mchezo mwingine wa kundi c.