Ivory Coast yaichapa Denmark 4-2

Mchezaji wa Ivory Coast Souleymane Coulibaly aliifungia timu yake magoli manne siku ya Alhamisi na kuonekana kama mmoja wa wachezaji nyota katika michuano inayoendelea nchini Mexico ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.

Haki miliki ya picha estadiodeportes.com
Image caption Souleymane Coulibaly

Denmark ndiyo waliotangulia kufunga magoli mawili lakini Ivory ikaweza kumakinika na kushinda mechi hio magoli 4-2.Kufikia wakati wa mapumziko Souleymane Coulibaly alikuwa amefunga magoli matatu na aliwaliza wachezaji wa Denmark alipoingiza goli la nne katika kipindi cha pili.

Ushindi huo katika uwanja wa Guadalajara umewapeleka Ivory Coast hadi nafasi ya pili kwenye kundi F, huku wakiwa na nafasi nzuri ya kufika hatua ya timu 16 bora,huku Denmark wakihitaji kufanya bidii katika mechi zao zilizobaki.

Coulibaly aendeleza rekodi bora

Coulibaly alifunga goli katika mechi ya ufunguzi ambako walifungwa magoli 2-1 na Australia na kwa jumla ya magoli matano,kufikia sasa yeye ndiye mfungaji bora wa michuano hio.

Haki miliki ya picha en.wikipedia.org
Image caption Uwanja wa Chuo Kikuu nchini Mexico unaotumika kwenye fainali ya FIFA U-17.

Katika kipindi cha pili,timu zote mbili ziliweza kuonesha mchezo wa kukomaa huku kila timu ikifanya mashambulizi, Coulibaly akiendelea kuwapa wakati mgumu wapinzani wake na Jean Kouassi akikosa magoli, lakini kwa mara nyingine ikawa ni Coulibaly aliyeingiza goli katika dakika ya 69.

Alipenya kwenye ngome ya ulinzi ya Denmark kabla ya kumchenga golikipa na kuingiza goli ndani upande wa kushoto.

Katika dakika za mwisho,alipumzishwa huku mashabiki wakimshangilia,kutokana na uhodari wake.

Mechi inayofuata Ivory Coast itacheza na Brazil huko huko Guadalajara na wana matumaini ya kuongoza kundi lao,na Denmark nayo inahitaji kuifunga Australia huko Queretaro ili waweze kupata nafasi ya kuingia kwenye raundi nyengine.