Kambi ya al-Shabab yashambuliwa

Wapiganaji wenye kuzingatia itikadi kali za kidini wa Somalia wameshambuliwa na helkopta za kigeni karibu na mji wa Kisimayo.

Hassan Yacqoub msemaji wa wapiganaji hao wa al Shabab amesema kuwa wapiganaji wao wawili waliokuwa wanapiga doria walishambuliwa jana jioni katika eneo la Qandal katika vitongoji vya mji huo wa Kisimayo. Amesema kuwa wapiganaji hao walilipiza kwa kuzilenga hizo helkopta zinazodhaniwa kuwa ni za Ufaransa ama Marekani. Kismayo ni ngome ya kundi la wapiganaji wa al-Shabab, kundi ambalo linauhusiano na Al-Qaeda na ambalo linashikilia sehemu kubwa ya kusini na kati ya Somalia.

Wakazi kutoka sehemu hiyo wameiambia BBC kuwa kuna kambi kubwa ya mafunzo ya al-Shabab katika eneo la Qandal kilomita 10 kusini mwa Kisimayo. Wanasema baadhi ya wanaofunzwa katika kambi hiyo ni wageni kutoka nchi za nje.

Wadadisi wanasema kuwa wapiganaji hao wa al-Shabab ni tisho kubwa kwa serikali iliyopo sasa ya muda ambayo tayari ni hafifu.

Kumekuwa na mashambulizi ya ndege za Marekani dhidi ya al-Shabab katika siku zilizopita na vile vile mwaka 2009 timu maalum ya Marekani ilifanikiwa kumuua Saleh Ali Saleh Nabhan mmoja wa viongozi wa al-Qaeda katika Afrika Mashariki.Marekani na Ufaransa zote zina kambi za kijeshi katika nchi jirani ya Djibouti.

Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na wanajeshi wa kudumisha amani wa Muungano wa Afrika, inadhibiti maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Mogadishu ulio kilomita 500 kaskazini mwa Kisimayo.

Somalia imekuwa bila serikali thabiti tangu kung’atuliwa Rais Siad Bare mwaka 1991, na tangu hapo kumekuwa na mvutano kati ya makundi mbalimbali yakizozania uwongozi.