Marekani yataka vikosi vya UN Abyei

Marekani imewasilisha rasimu kwa Umoja wa Mataifa ikitaka walinda amani 4,000 kupelekwa kwenye eneo linalozozaniwa la Abyei.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wa kutunza amani wa UN

Eneo la Abyei limo kwenye mpaka wa Sudan Kaskazini na Sudan Kusini.

Kumekuwa na makabiliano makali kwenye eneo hilo katika kipindi cha majuma kadhaa yaliopita lakini pande zote mbili zilitia saini mkataba mapema wiki hii ili kuondoa majeshi.

Pande zote mbili, serikali ya Kaskazini na Kusini, zimekubali kuruhusu walinda amani wa Ethiopia kushika doria katika eneo hilo.

Susan Rice amesema mkataba wa kuwanyang'anya silaha wapiganaji ni hafifu na kuongezea kwamba kupelekwa kwa walinda amani 4,200 kutahakikisha kuwa mpango huo unatekelezwa haraka.

Mzozo wa umiliki

Kila upande unatarajia kuwa eneo la Abyei litajumuishwa kuwa lao pindi tu Sudan Kusini itakapotangaza uhuru wake tarehe 9 Julai.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mama mmoja akitembea katika bara bara za mji wa Abyei

Chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 yaliomaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, eneo la Abyei lilipewa uwezo wa kipekee, na mwaka 2008, kukaundwa kamati ya kuliongoza.

Kulikuwa na mpango wa kufanyika mchkato wa kupiga kura ya maoni mwezi Januari kuhusu mustakabali wa eneo la Abyei lakini upigaji kura ukaahirishwa.

Hali ya taharuki imekuwa ikipanda tangu Mei 21, wakati serikali ya Khartoum ilipotuma majeshi yake kwenye eneo hilo na kuzua hisia kali kutoka kwa jamii ya kimataifa kwa kuhofia kuwa hatua hio ingezua tena mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Umoja wa Mataifa unasema takriban watu 10,000 wametoroka kutoka eneo hilo.