Wanasoka maarufu wajiunga na waasi Libya

Kundi la wachezaji soka 17 wa Libya wametangaza kujiunga na waasi.

Image caption Juma Gtat, golikipa wa timu ya taifa ya Libya na kocha wa al-Ahly, Adel Issa

Ni pamoja na golikipa wa taifa hilo, Juma Gtat, wachezaji wengine watatu wa timu ya taifa, na kocha wa timu kuu ya Tripoli al-Ahly, Adel bin Issa.

Bw Gtat na Bw Issa walitangaza kuasi kwao kwa BBC wakati kukifanyika mkutano nyakati za usiku kwenye eneo lililoshikiliwa na waasi la milima ya Nafusa magharibi mwa Libya.

Hatua hiyo inatokea baada ya maafisa wa jeshi nao kuasi.

Pigo kubwa kwa Kanali Gaddafi

Katika hoteli mjini Jadu mwandishi wa BBC Mark Doyle alikutana na golikipa Juma Gtat akiwa amepumzika chumbani kwake.

" Namwambia Kanali Gaddafi atuache na aturuhusu tuunde Libya huru," Alisema wakati wakikaa juu ya kitanda cha hoteli mbele ya wachezaji wengine.

Aliongeza huku akicheka, " Kwa hakika natamani aondoke duniani kabisa."

Kwa nchi hiyo iliyopo kaskazini mwa Afrika yenye wapenzi tele wa soka, kuasi huko kwa hakika ni pigo kubwa kwa Kanali Gaddafi. Lakini wakati wote amekuwa akipambana na shinikizo, la kisiasa na kijeshi, la kuondoka madarakani.

Na bado ana nafasi kubwa katika maeneo mbalimbali ya vita nchini humo.

Huko, katika eneo la milima magharibi mwa nchi hiyo linaloshikiliwa na waasi, huku Misrata ikiwa imezingirwa kati kati, na pia upande wa mashariki, kiongozi huyo wa Libya ana idadi kubwa ya silaha nzito.

Wengi wa waasi wana bunduki ndogo, na kwa baadhi , wana bunduki za zamani.

Roketi za masafa marefu na makombora kwa agizo la Kanali Gaddafi kunamaanisha kuwa anaweza kuwashambulia waasi ipasavyo.

Bw Issa, alimwambia Doyle aliamua kwende kwenye eneo la milima hiyo "kutuma ujumbe kuwa Libya inahitaji umoja na kuwa huru".

"Natamani siku moja niamke asubuhi na nikute Gaddafi hayupo tena," Aliongeza.