Wen Jiabao azuru Uingereza

Wen Jiabao Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wen Jiabao

Waziri Mkuu wa Uchina, Wen Jiabao yuko Uingereza kwa ziara ya siku tatu, ili kuimarisha uwekezaji wa Uchina katika makampuni ya Uingereza.

Wakati wa ziara hiyo, wanaharakati wanaopigania haki za kibinaadamu, wanajaribu kufanya kampeni ya kuonesha hatua zinazochukuliwa na Uchina kuwazima wapinzani wa serikali ya nchi hiyo.

Wen Jiabao alipowasili katika uwanja wa ndege wa mji wa Birmingham, Uingereza, ilitangazwa mpigania haki za kibinaadamu maarufu wa Uchina, Hu Jia, ameachiliwa huru baada ya kifungo cha miaka mitatu na nusu kwa usaliti.

Siku chache zilizopita, msanii Ai Weiwei piya alifunguliwa.

Uingereza bado ina wasiwasi juu ya hali ya haki za kibinaadamu Uchina, na swala hilo linatarajiwa kutajwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron atapokutana na mwenzake wa Uchina, hapo kesho.

Lakini lengo hasa la ziara ya Bwana Wen ni kuimarisha uhusiano katika biashara, uchumi na siasa.

Bwana Wen atazuru kiwanda cha kutengeneza magari aina ya MG, Longbridge, karibu na Birmingham, ambacho sasa kinamilikiwa na kampuni ya Uchina.

Bwana Wen anaanza ziara yake kwa kuzuru pahala alipozaliwa mwandishi wa kale wa Uingereza wa michezo wa kuigiza, tamthilia, William Shakespeare huko Stratford-upon-Avon.

Inaarifiwa kuwa Bwana Wen Jiabao ni mshabiki mkubwa wa Shakespeare.