Ocean View yaingia robo Fainali

Timu ya Zanzibar Ocean View imekuwa ya kwanza kujihakikishia kuingia hatua ya Robo fainali katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama kombe la Kagame baada ya kushinda mechi ya pili mfululizo kwa kuichapa Red Sea ya Eritrea 2-0 katika mchezouliocheza kwenye uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Tanzania.

Haki miliki ya picha
Image caption Kombe la Kagame

Katika mchezo wa kwanza ulichezwa siku ya ufunguzi wa michuano hiyo Jumamosi Zanzibar Ocean View waliilaza Etincelles ya Rwanda 3-2.

Wakiwa wenye kujiamini Zanzibar Ocean View walipata goli la kwanza katika dakika ya 35 kipindi cha kwanza goli lililofungwa na Suleiman Haji kwa shuti kali baada kupokea pasi kutoka kwa Mohamed Hamduni hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Zanzibar Ocen View ilitoka kifua mbele kwa 1-0. Kipindi cha pili kilikuwa cha mshikemshike lakini ni Zanzibar Ocean View walioonekana kuutawala zaidi mchezo huo ambapo katika dakika ya 86 Said Rashid alimalizia karamu ya leo kwa kufunga goli la pili hadi mpira unamalizika matokeo yalikuwa 2-0. Katika mchezo huo Aron Zakarias wa Red Sea alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia faulo mbaya Salum Shebe wa Zanzibar Ocean View.

Katika mchezo wa pili timu ya Vital’o FC ya Burundi imejiweka katika mazingira mazuri ya kuingia hatua ya Robo Fainali baada ya kuifunga timu ya Entincelles ya Rwanda kwa magoli 3-1. Katika mchezo wa awali timu hiyo ya Vital’o FC ilitoka sare ya kutofungana na timu ya Simba ya Tanzania. Magoli ya Vital’o FC yamefungwa na Steive Nzigamasabo, Stanley Minzi na Miami Mbakiye huku goli pekee la Entincelles likifungwa na Claver Muhire Kwa matokeo hayo timu ya Zanzibar Ocean View ndio wanaoongoza kundi A wakiwa na jumla ya pointi 6 baada ya kushinda mechi zote mbili huku Vital’o ya Burundi ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 4.

Timu ya Simba ya Tanzania ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi moja wakati timu za Entincelles ya Rwanda na Red Sea ya Eritrea hazina pointi.