Shambulio la bomu laua 25 nchini Nigeria

Shambulio hilo lilitokea muda wa saa kumi na moja jioni watu wakiwa wanastarehe kwenye baa moja mjini Maiduguri.

Kulingana na duru za kiusalama na watu walioshuhudia, watu wanashukiwa kuwa wafuasi wa kundi la boko haram walifika katika ukumbi huo wa starehe wakiwa wamebebwa kwenye pikipiki, kisha wakarusha mabomu kwenye baa hiyo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kundi la boko haram linadaiwa kutekeleza shambulio hio mjini Maiduguri

Inasemekana kuwa walirusha mabomu matatu kwenye klabu hicho cha pombe. Milipuko iliotokea imesababisha vifo vya watu 25 na wengine wengi kujeruhiwa.

Kufikia usiku wa manane, wafanyikazi wa idara ya huduma za dharura na wazima moto bado walikuwa kwenye eneo la tukio katika harakati za kuokoa majeruhi na kukabiliana na moto.

Ingawa kundi la boko haram halijakiri kutekeleza shambulio hilo, polisi wanahisi kuwa huenda limehusika.

Kundi hilo lenye itikadi kali za dini ya kiisalmu linalopinga elimu ya kisasa, limekuwa likitekeleza mashambulio ya bomu kaskazini mwa Nigeria, ambako pia ni ngome yake.

Boko haram walikiri kuhusika na shambulio la bomu kwenye makao makuu ya polisi mjini Abuja wiki mbili zilizopita.

Tangu kiongozi wa kundi hilo Mohammed Yusuf afe akiwa chini ya ulinzi wa polisi mwaka wa 2009, Kundi hilo lilitangaza vita dhidi ya kikosi hicho na limekuwa likawashambulia kaskazini mwa Nigeria.

Nia ya boko haram ni kuwa sheria za kiislamu zitumike kote nchini Nigeria.

Wafuasi wake pia wamekuwa wakishambulia viongozi wa kitamaduni na maimamu wenye misimamo ya wastani.

Rais Goodluck Jonathan anataka serikali ifanye mazungumzo na kundi hilo ambalo sasa linatishia kuwa changamoto kubwa kwa utawala wake kando na wapiganaji walioko kwenye jimbo la Niger Delta kunapozalishwa mafuta.

Hata hivyo wadadisi wa masuala ya kiusalama wanasema mazungumzo na kundi hilo yatakuwa magumu kuanzisha kwani, uongozi wa Boko haram hauna mfumo wa kuaminika na kwa sasa haijulikani nani ndiye amiri.