Aliyekuwa rais wa Zambia Chiluba azikwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Marehemu Fredrick Chiluba na mkewe Regina mjini Lusaka

Aliyekuwa Rais wa Zambia Frederick Chiluba amezikwa kwenye mji mkuu, Lusaka, kufuatia kifo chake wiki moja iliyopita.

Mamia ya waombolezaji, walioongozwa na Rais Rupiah Banda, walihudhuria mazishi hayo.

Bw Chiluba alifariki dunia nyumbani kwake mwishoni mwa juma- sababu ya kifo chake hakijtangazwa kwa umma mpaka sasa.

Aliiongoza Zambia kwenye demokrasia kwa kuanzisha vyama vingi mwaka 1991, lakini urais wake uligubikwa na madai ya rushwa.

Mwandishi wa BBC Mutuna Chanda mjini Lusaka alisema Wazambia wengi wanaamini udhaifu wa Bw Chiluba usiangaliwe sana na badala yake akumbukwe kwa kumaliza utawala wa chama kimoja.

Amezikwa pembeni mwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Levy Mwanawasa, katika makaburi maalum kwa ajili ya Marais.

Bw Mwanawasa, aliyemrithi Bw Chiluba, alifariki dunia mwaka 2008.

Maelfu ya watu walishuhudia mazishi ya Bw Chiluba kupitia televisheni ya taifa na kwenye skrini kubwa ziliozwekwa nchini kote.

Viongozi wakuu kutoka nchi za kigeni waliohudhuria mazishi hayo ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jospeh Kabila na waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai.