Nato wafaulu kudhibiti shambulio kabul

Yamkini watu kumi na wawili wamefariki baada ya washambuliaji wakujitoa mhanga kuvamia hoteli ya kifahari ya Intercontinental mjini Kabul, Afghanistan.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wakuu wa mikoa walikuwa wanafanya mkutano wakati wa shambulio hilo

Baada ya makabiliano ya saa tano katika hoteli hiyo, hatimae wanajeshi wa Nato wakitumia helikopta walifaulu kuwauwa wanamgambo wanne ambao walikuwa wamepanda kwenye paa la hoteli hiyo.

Kulingana na msemaji wa jeshi la Nato kanali Tim James, wanamgambo hao walikuwa wamevalia fulana zilizokuwa na mabomu.

Hoteli hiyo ya Intercontinental ni maarufu sana miongoni mwa raia wa kigeni, lakini wote walikuwa salama hata baada ya shambulio hilo.

Kulingana na maafisa wa uslama wa serikali ya Afghanistan, wamshambuliaji sita walivamia hoteli hiyo lakini wote sasa wameuawa.

Viongozi wa kundi la wanamgambo wa Taleban wamedai kuhusika na shambulio hilo ambalo lilitokea wakati wageni wengi walikuwa wanapata chakula chao cha jioni.

Msemaji wa idara ya usalama wa ndani nchini humo Siddiq Siddiqi amesema waliouawa ni raia wa Afghanistan na watu wengine nane walijeruhiwa katika tukio hilo.

Wakuu wa usalama wanasema huenda wanamgambo hao walikuwa wamelenga kushambulia mkutano wa wakuu wa mikoa uliokuwa ukiendelea kwenye hoteli hiyo.

Hoteli ya Intercontinental ni maarufu kuwa na usalama mzuri zaidi nchini Afghanistan.