Yanga yairarua Elman ya Somalia

Timu ya Elman ya Somalia imekuwa timu ya pili kuyaaga mashindano Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame Cup baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-0 kutoka klabu ya Yanga ya Tanzania katika mechi ya kundi B iliyochezwa katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam Tanzania.

Image caption Elman ya Somalia

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa timu hiyo ya Elman kukubali kipigo ambapo katika mechi ya awali ilipocheza na Bunamwaya ya Uganda timu hiyo ilifungwa 4-1. Magoli ya Yanga yalifungwa na Davies Mwape katika kipindi cha kwanza huku la pili likifungwa na Hamis Kiiza katika dakika za majeruhi. Katika mechi nyingine iliyochezwa katika uwanja huo huo wa Taifa Dar es Salaam, timu ya Bunamwaya ya Uganda imetoka sare na timu ya Al Mereikh ya Sudan 1-1 Kwa matokeo hayo timu ya Bunamwaya ya Uganda ndio inayoongoza kundi B ikiwa na pointi nne sawa na Yanga ya Tanzania lakini ikiwa imeiizidi Yanga kwa idadi ya magoli, Yanga ya pili na Al Mereikh Sudani nafasi ya tatu ikiwa na pointi 2 huku Elman ya Somalia ikishika mkia kwani haina pointi hata moja hadi sasa. Matokeo mengine ni ya kundi C ya mechi zilizochezwa katika kituo cha Morogoro kilichopo Mashariki mwa Tanzania kunakoendelea mashindano hayo ambapo timu ya Ulinzi ya Kenya imeinyeshea mvua ya magoli timu ya Port ya Djibout kwa jumla ya magoli 9 – 0. Na katika mchezo wa pili wa kundi C uliochezwa huko huko Morogoro timu ya APR ya Rwanda imekubali kipigo kutoka kwa St. George ya Ethiopia cha magoli 3-1. Michuano hiyo inaendelea siku ya Ijumaa katika kituo cha Dar es Salaam ambapo katika mechi ya kwanza Vital’o ya Burundi itamenyana na Red Sea ya Eritrea huku katika mechi ya pili Simba ya Tanzania itaumana vikali na Etincelles ya Rwanda.