Amri Nigeria kuhusu maeneo ya burudani

Mashambulizi ya bomu Nigeria Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mashambulizi ya bomu Nigeria

Serikali ya Nigeria imetoa amri na maagizo ya saa za kufungwa vilabu, baa na majumba ya cinema katika mji mkuu wa Abuja, hatua hii inakuja wiki mbili baada ya mji wa Abuja kushambuliwa kwa mabomu.

Maeneo haya ya burudani kwa sasa yatalazimika kufunga shughuli zake kufikia saa nne za usiku za Nigeria. Nayo mabostani ya umma yanayotembelewa na watoto, sasa yanapaswa kufunga milango yake saa kumi na mbili jioni.

Watu wanane walikufa katika mashambulizi ya hivi majuzi yaliolenga makao makuu ya Polisi. Mashambulizi hayo yalitekelezwa na kikundi cha wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali cha Boko Haram.

Kikundi hicho pia kinashutumiwa kwa mashambulizi ya Jumapili dhidi ya maskani moja ya wazi ya kunywa pombe katika eneo la Maiduguri.

Kikundi hicho ambacho kawaida hushambulia na hasa kulilenga jimbo la kaskazini mashariki la Borno kinasema kinapigania utawala wa Kiislamu na kinafanya kampeini dhidi ya shughuli zote za kisiasa na kijamii zilizo na uhusiano ama mvuto wa kimagharibi.