Radi yasababisha vifo zaidi Uganda

Nchini Uganda radi imesababisha vifo vya wanafunzi 18 na wengine 50 kujeruhiwa ilipopiga shule moja ya msingi magharibi mwa nchi hiyo.

Image caption Ramani ya Uganda

Msemaji wa polisi Judith Nabakooba ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanafunzi wakike 15 na wakiume watatu walikufa jana jioni katika shule ya msingi ya Runyanya wilaya ya Kiryandongo.

Wasiwasi kuhusu mfululizo wa radi kali zinazoipiga Uganda kwa wakati huu umesababisha wabunge nchini humo kulijadili suala hili bungeni.

Wiki iliyopita watu wasiopungua 28 waliuawa na radi na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa mwanasayansi anayeshughulika na masuala ya hali ya hewa kutoka Uganda Kiza Aderi, ukosefu wa vifaa vya kukabiliana na radi katika majengo kadhaa huenda ikiwa ni moja wapo ya sababu zinazosababisha watu kuuawa na radi.

Kamanda wa polisi wa wilaya ya Kiryandongo Patrick Byaruhanga ameliambia gazeti la taifa la New Vision kuwa radi hiyo ilipiga karibu saa kumi unusu jioni za Uganda wakati wanafunzi walikuwa bado madarasani wakisubiri mvua itue kabla ya kwenda nyumbani.

Msemaji wa polisi amesema baadhi ya waliopata majeraha makubwa wamepelekwa katika hospitali ya Mulago katika mji mkuu wa Kampala kilomita 200 kusini mashariki ya Uganda.

Nchi ya Uganda inashuhudia kipindi cha mvua na dhoruba kali na visa vya vifo kutokana na radi vimewatia watu wengi wasiwasi.