Mawaziri wa Misri wanabadilishwa

Waziri Mkuu wa Misri ameanza kubadilisha baraza lake la mawaziri, kutokana na malalamiko yanayozidi kuwa marekibisho ya kisiasa yanakwenda taratibu mno.

Mabadiliko hayo yalitangazwa na Waziri Mkuu, Essam Sharaf, huku maandamano yanaendelea mjini Cairo na miji mengine dhidi ya serikali.

Kutokana na chagizo za maandamano, waziri mkuu wa Misri ameanza kutekeleza yale yanayotarajiwa kuwa mabadiliko makubwa katika serikali yake.

Mabadiliko hayo yamechukua zaidi ya wiki, ambayo ni ishara kuwa waziri mkuu anakabili upinzani ndani ya halmashauri ya kijeshi inayoongoza nchi.

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje, ambaye anahusishwa na uongozi wa zamani, amejiuzulu.

Vyombo vya habari vya taifa vinasema mawaziri kama 15 wanatarajiwa kubadilishwa, katika jaribio la kukata kabisa fungamanisho na serikali ya zamani ya Rais Mubarak.

Manaibu wawili wa waziri mkuu wameteuliwa, mmoja miaka 74, na mwengine miaka 75.

Wakati huo huo jeshi limesema litapunguza kutumia mahakama ya kijeshi, ambayo yamelaumiwa vikali na upinzani.

Lakini jenerali mmoja aliyekwenda kuonana na waandamanaji katika Medani ya Tahrir alizomewa na kurushiwa viatu, na ikambidi kuondoka. Kwenye tovuti ya Facebook, waziri mkuu alisema mabadiliko ya mawaziri ni hatua ya mwanzo tu.

Aliwaambia Wamisri "najitahidi sana kutimiza matakwa yenu".