Watu maelfu wanatafuta chakula Somalia

Wakati ukame unaendelea Afrika Mashariki, Shirika la Kimataifa la Matibabu, MSF, linasema kuwa limeanza kuona makambi ya watu maelfu kadha ndani ya Somalia kwenyewe.

Inakisiwa kuwa ukame huo umeathiri watu milioni 10, na watu wanatembea kilomita mia kadha kutafuta chakula.

Msemaji wa MSF katika Pembe ya Afrika, Joe Belliveau, aliiambia BBC kwamba idadi ya watu katika kambi moja imeongezeka mara dufu katika siku chache:

"Tumeona watu wakiongezeka katika kambi moja.

Juma lilopita tu, kambi hiyo ilikuwa na familia kama mia tatu, na katika siku chache, idadi imezidi kufikia familia mia nane, na watu wanaendelea kuhama.

Ndio sababu unaona kuna watu wanakimbilia Ethiopia na wengine wanahama ndani ya Somalia kwenyewe, kwa sababu hawana cha kutegemea.

Wanabeba virago na kuhama".

Na afisa wa Shirika la huduma za dharura la Umoja wa Mataifa leo amezuru Dollo Somalia, mpakani baina ya Somalia na Ethiopia.

Abdulrazak Atosh wa BBC alikuwa katika msafara huo, na anasema ameona watu waliodhoofika hasa akina mama na watoto wao, ambao walimuelezea kuwa walibidi kuwaacha watoto wao wengine njiani, kwa sababu watoto walikuwa wamedhoofika sana na hawakuweza kutembea.

Mashirika ya misaada katika mji wa Dolo-Somalia piya hawakuwa na chakula cha kutosha kuwasaidia wakimbizi hao.