Syria inafanya kongamano la taifa

Mkutano wa majadiliano kuhusu taifa unafanywa leo nchini Syria katika mji mkuu, Damascus, ili kuridhia malalamiko ya watu waliofanya maandamano yaliyoendelea kwa miezi kadha dhidi ya Rais Bashar al-Assad.

Kongamano hilo la siku mbili, litajumuisha wajumbe wa chama tawala cha Baath na wale wanaokipinga, na litajadili uwezekano wa kufanya mabadiliko kadha ya kisiasa.

Vyombo vya habari vya taifa vya Syria vinasema kongamano hilo la mwanzo litahudhuriwa na wajumbe 200, pamoja na waakilishi wa chama tawala cha Baath na washirika wake, upinzani, watu wanaojitegemea, wasomi na vijana.

Maswala kadha yatajadiliwa pamoja na uwezekano wa kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na sheria mpya kuhusu vyombo vya habari.

Mkutano huo utaweka utaratibu na muda wa kutekeleza hayo.

Rais Bashar Al Assad alipotangaza mazungumzo hayo mara ya mwanzo mwezi uliopita, alisema anataka mpango uliokamilika, na ambao utashughulika na maswala mbali mbali yanayokabili watu wa Syria

Kukubalika kwa majadiliano hayo ya taifa, kutategemea wajumbe gani wa upinzani watashirikishwa.

Maandamano yaliyofanywa Ijumaa yalikuwa na nembo "hakuna mazungumzo Ijumaa".