Mchochezi wa chuki Ivory Coast asakwa

Nchi ya Ivory Coast imewasilisha waranti ya Kimataifa ya kutaka akamatwe aliyekuwa kiongozi wa vijana wanamgambo wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Laurent Gbagbo, ambaye tangu mwezi April amekuwa akitafutwa.

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Goude

Mwendesha mashtaka amesema kuwa Charles Ble Goude anatakiwa kwa kuchochea malumbano ya kikamila na kuchukia wageni, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Reuters.

Charles Goude anakumbukwa kwa hotuba zake za uchochezi alipowachagiza vijana kwa maelfu kujiunga na jeshi katika siku za mwisho mwisho za mapambano ya kupinga matokeo ya Uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Novemba.

Bw. Gbagbo aliondolewa madarakani kwa nguvu baada ya kukataa kukubali matokeo ya kushindwa kwenye Uchaguzi huo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Laurent Gbagbo

Kadri ya watu 3,000 waliuawa kabla ya Bw.Gbagbo kukamatwa mnamo mwezi April.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu 3000 waliuawa
Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Allasane Outtara

Uchaguzi mkuu wa Ivory Coast ulisimamiwa na Umoja wa Mataifa na kusema kuwa mshindi alikuwa ni kiongozi wa upinzani Bw Alassane Ouattara, ambaye baada ya kuondolewa Gbagbo alikula kiapo na kushika hatamu za uongozi kama Rais wa Ivory Coast.

Kifungo cha Nyumbani Bw.Ble Goude, ambaye aliorodheshwa katika vikwazo vya Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2006 kwa tuhuma za kuchochea mashambulizi dhidi ya vikosi vya kuhifadhi amani vya Umoja wa Mataifa, amekuwa akisakwa tangu kukamatwa kwa Bw. Laurent Gbagbo.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu Bw.Goude ameonekana nchini Benin na Ghana pia.

Waranti za kukamatwa kwa washukiwa kadhaa walio kimbia zimeisha tolewa na mwana sheria Simlice Kouadio Koffi.

Bw.Gbagbo alimtangaza Bw. Ble Goude kama Waziri wake wa Vijana baada ya Uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba alipokanusha matokeo ya kura.

Katika kipindi cha miezi menne iliyofuata Uchaguzi, wafuasi wengi wa kundi la Bw.Ble Goude lililojulikana kama Young Patriots lilipewa silaha za kupigana.

"shirika la Habari, Reuters limearifu kuwa ''Kwa majuma kadhaa, watu hao walinadi chuki na shinikizo za kuwatenga na kuua wageni pamoja na kutenda maovu ya kila aina dhidi ya wananchi wenzao,alisema Mwanasheria mkuu.

Warranti nyingine imewasilishwa kwa kutaka akamatwe aliyekuwa msemaji wa Bw.Gbagbo, Ahoua Don Mello, Waziri wa zamani Philippe Attey na aliyekuwa Balozi wa nchi nchini Israel, Raymond Koudou Kessie.

Serikali ya Bw.Ouattara imeahidi kukomesha tabia kutowaadhibu wahalifu ingawaje ni wafuasi wa Gbagbo pekee ndiyo waliokamatwa hadi sasa licha ya utafiti wa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kuonyesha kuwa pande zote mbili zilishiriki vitendo vinavyokiuka haki za utu.

Hadi sasa Bw.Gbagbo hajafunguliwa mashtaka na bado amezuiliwa katika nyumba moja iliyo katika sehemu ya kaskazini mwa nchi.

Uchaguzi uliofanywa nchini Ivory Coast wakati huo ulikusudia kuondoa msitari uliowekwa kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002-03 ikiiacha nchi imegawika mara mbili.