Sudan si nchi kubwa tena Afrika

Sudan Kusini itakuwa taifa huru siku ya Jumamosi, baada ya vita vya miaka mingi na upande wa kaskazini.

Hivi sasa Sudan imechapisha takwimu mpya kuhusu kitakachosalia katika taifa hilo la zamani.

Takwimu hizo ni pamoja na ramani ya taifa jipya ikionyesha eneo la mpaka unaozozaniwa kuwa sehemu ya Sudan.

Image caption Sudan

Mwandishi wa BBC James Copnall akiwa Khartoum amesema Sudan itapoteza hadhi yake ya kuwa nchi kubwa ya Afrika kupita zote pale kusini itakapojitenga.

Pia itapoteza robo tatu ya utajiri wake wa mafuta. Lakini Khartoum inajaribu kutoa ujumbe wa matumaini mema.

Serikali hiyo imechapisha kitabu cha ufafanuzi kikiambatana na CD, kiitwacho Sudan - nchi yenye fursa nyingi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Omar al-Bashir na Salva Kiir

Jumla ya wakaazi watakua zaidi ya millioni 33 , huku pato la taifa likiwa ni takriban dola za kimarekani 2400, kwa mujibu wa kitabu hicho.

Pia kitabu hicho kinatilia mkazo utajiri kama dhahabu na chuma pamoja na mchango wa akina mama katika taifa hilo.

Ramani rasmi ya nchi hiyo imezusha utata kwani inajumuisha pia mkoa unaozozaniwa wa Abyei, ulio kwenye mpaka kati ya Sudan na nchi mpya ya Sudan Kusini.

Hadhi ya Abyei bado haikukubaliwa. Hivi sasa iko chini ya utawala wa Khartoum, baada ya majeshi ya Sudan kulitwaa eneo hilo mwezi Mei.

Bado majadiliano yanaendelea kuhusu eneo hilo liwe upande gani ,ingawa kwa sasa lina hadhi maalum na kaskazini.

Juhudi za serikali ya Khartoum kuzungumzia mipango yake ya siku zijazo inakuja katika wakati ambapo hali ya wasiwasi inazidi kuendelea.

Kupotelewa hasa na utajiri wa mafuta ya kusini kutakuwa pigo kubwa kwa uchumi wa Sudan.