Timu za Soka za Cameroon na Afrika Kusini zimefuzu kwa fainali za Michezo ya 10 ya bara la Afrika

Timu za Soka za Cameroon na Afrika Kusini zimefuzu kwa fainali za Michezo ya 10 ya bara la Afrika itakayofanyika mjini Maputo, Msumbiji mwezi Septemba.

Cameroon iliifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mabao 3-0 mjini Younde, na hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.

Katika mechi iliyomalizika muda mfupi uliopita MJINI Harare Afrika Kusini imefuzu licha ya kufungwa bao moja kwa bila na wenyeji Zimbabwe. Afrika Kusini ilikuwa imepata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza.

Sasa hivi mjini Kumasi wenyeji Ghana wanachuana na Nigeria kutafuta MOJAWAPO YA NAFASI MBILI zilizosalia.

Ghana wanahitaji kubirua ushindi wa Nigeria wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza majuma mawili yaliyopita, na nahodha wao Samuel Inkoom anasisitiza hilo watatekeleza.

Nafasi ya mwisho itafahamika baadaye Senegal na Guinea zitakapochuana mjini Dakar, Gunea wakiwa na nguvu ya ushindi wa bao moja kwa bila kutokana na mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita.

Uganda imeshafuzu za michezo hiyo baada ya jirani zao Kenya kujiondoa kushiriki mechi ya marudiano iliyopangiwa kuchezwa mjini Kampala.

Wenyeji Msumbiji wameshafuzu pamoja na Misri na Madagascar.

Timu zinazoshiriki fainali hizo ni za wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23.

Michezo ya 10 ya bara la Afrika itafanyika mjini Maputo tarehe 3-18 mwezi Septemba.