Murdoch akiri udhaifu wa vyombo vyake

Tajiri mkubwa wa vyombo vya habari duniani, Rupert Murdoch, ameiambia kamati ya bunge la Uingereza kuwa hahusiki na kashfa ya udukuzi katika moja ya magazeti yake la News of the World ambalo kwa sasa halipo tena.

Image caption Rupert Murdoch

Hata hivyo, Bwana Murdoch amesema hakujua kilichokuwa kikiendelea katika gazeti hilo na alipotoshwa na watu aliowaamini. Amesema ameshtushwa na kuaibishwa na kashfa hiyo alipotambua kuwa News of the World lilihusika na udukuzi wa msichana wa shule aliyekuwa ameuawa.Murdoch ameomba radhi kwa kitendo hicho.

Wakati huo huo kamati ya bunge la Uingereza imetoa taarifa kali juu ya polisi walivyoshindwa kuchunguza kashfa ya udukuzi wa simu uliofanywa na waandishi wa habari katika moja ya magazeti ya Bwana Murdoch.

Shirika la News International la tajiri Rupert Murdoch lililazimika kufunga gazeti linalosomwa na watu wengi zaidi Uingereza la News of The World, baada ya kugunduliwa vitendo vya wafanyakazi wake kunasa mawasiliano ya simu za watu.

Katika historia yake ndefu gazeti hilo lilichapisha habari nyingi za kufichua udanganyifu na makosa mengine ya watu matajiri na wenye ushawishi mkubwa katika jamii, pamoja na habari za siri za watu maarufu kama vile wachezaji , waimbaji na kadhalika.