Simba yatinga fainali

Simba
Image caption Simba ya Tanzania

Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania imeingia fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kagame Cup baada ya kuisambaratisha timu ya Al Mereikh ya Sudan kwa njia ya mikwaju ya penati 5 -4.

Mikwaju ya penati ilifuatia baada ya dakika 90 na hatimaye dakika 30 za nyongeza kutozaa matunda katika mechi ya kukata na shoka iliyochezwa katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam. Huenda sifa na pongezi zikamiminika kwa mlinda mlango wa Simba Juma Kaseja ambaye ndiye aliyewapeleka fainali baada ya kuokoa penati ya mwisho iliyopigwa na Al Mereikh. Timu hizo zilingia katika hatua ya kupigiana penati baada ya kumaliza dakika 120 zikiwa zimefungana 1 - 1. Simba sasa itacheza fainali siku ya jumapili na mshindi wa mechi kati ya Yanga ya Tanzania na St. George ya Ethiopia ambaye atajulikana siku ya Ijumaa. Yanga na St. George zitamenyana siku ya Ijumaa katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya michuano hiyo. Kwa matokeo hayo Al Mereikh sasa itacheza mapema siku ya jumapili kutafuta nafasi ya mshindi wa tatu ya michuano hiyo ya CECAFA na timu itakayoshindwa kuingia fainali kati ya Yanga ya Tanzania na St. George ya Ethiopia.