Mlipuko wasababisha maafa Cameroon

Ramani ya Cameroon
Image caption Ramani ya Cameroon

Wafanyibiashara haramu wa mafuta ya petroli nchini Cameroon wamekufa baada ya lori kubwa lililokuwa na petroli kinyume na sheria kulipuka kaskazini mwa mji wa Dembo unaopakana na Nigeria.

Moto ulizuka saa nne za usiku mara tu baada ya lori hilo kuvuka mpaka.

Mtu mmoja aliyeshuhudia amesema ameona maiti za watu sita zilizoteketea kiasi cha kutotambulika, maiti hizo zilikuwa pamoja na ile ya Dereva wa lori hilo.

Serikali ya Nigeria inachangia sana katika suala la mafuta, jambo ambalo linayafanya mafuta kutoka Nigeria kuonekana kama kivuta faida kwa wafanyibiashara haramu wanayoyapeleka nchini Cameroon.

Haijulikani bado nini kilichosababisha mlipuko huo, lakini taarifa zasema ajali kama hizo ni kawaida.

Mwezi jana Cameroon ilipiga marufuku safari za usiku katika barabara ambazo hazijatiwa lami ili kupunguza ajali zinazosababishwa na madereva walevi.

Mwandishi wa BBC Randy Joe Sa'ah akiwa katika mji mkuu wa Yaounde, anasema kuwa mafuta ya Nigeria yanayojulikana kama "Zoa -Zoa" yanauzwa kila pembe ya nchi hiyo. Mwandishi huyo ameongeza kusema kuwa bei yake ni nafuu na yanapatikana kwa urahisi katika mji mkuu wa jimbo Garoua ilikinganishwa na yale mafuta ambayo husafishwa kusini mwa Cameroon.

Biashara haramu imenawiri na inawavutia wengi kati ya vijana wa eneo hilo ambao hawana ajira.

Haman Oumar, afisa wa serikali anaehusika na masuala ya biashara, anasema watoto wengi wameacha kwenda shule na kujiingiza katika biashara hiyo.

Mwandishi wetu anasema baadhi ya vijana huvuka mipaka kwa kutumia baiskeli zao kwenda kuchukuwa mitungi ya petroli ngambo ya pili.

Afisa msimamizi wa eneo hilo la Benue anasema tukio la Dembo, kilomita 35 kaskazini-magharibi mwa Garoua, linaonesha wazi sababu ya kuimarisha vita dhidi ya biashara haramu ya mafuta. Mwezi November mwaka jana afisa huyo alianzisha kampeini ya kukabiliana na biashara hiyo.

Lakini wafanyibiashara wanasema serikali inaitegemea biashara hiyo haramu kwa mapato yanayotokana na ushuru unaotozwa bidhaa kutoka nje licha ya kuwa ni bidhaa zinazoingizwa nchini kinyume na sheria.