Strauss-Kahn anakabiliwa na shutuma zingine

Dominique Strauss-Kahn
Image caption Dominique Strauss-Kahn

Mwandishi mmoja raia wa Ufaransa ambaye anadai alishambuliwa na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la fedha duniani, Dominique Strauss-Kahn, miaka tisa iliopita anajiandaa kuwasilisha kesi dhidi yake.Wakili wa mwandishi huyo,Tristane Banon, amesema atawasilisha madai ya kujaribu kubaka dhidi ya Strauss-Kahn.

Saa kadhaa baada ya mwandishi huyo kutangaza azimio lake,Bwana Strauss Kahn alimuagiza wakili wake kumshtaki kwa kile alichokitaja kama kuanzisha madai ya uongo.

Ijumaa iliopita,Bwana Strauss-Kahn aliondolewa masharti aliyokuwa amewekewa baada ya kutoa dhamana huko New York. Hii ni baada ya mwendesha mashtaka katika kesi hiyo kukiri kwamba ana wasiwasi kuhusu uaminifu wa mwanamke mmoja anayedai kuwa Strauss-Kahn alijaribu kumbaka.Amekana madai hayo.

Bado kesi inaendelea,lakini kuna matumaini nchini Ufaransa kuwa kesi hio huenda ikatupiliwa mbali.

Mwezi Mei,mwandishi huyo alisema kwamba kufuatia kesi iliyowasilishwa dhidi ya Bwana Strauss-Kahn huko New York na mfanyakazi wa hoteli moja, hatimaye pia yeye angeweza kuwasilisha kesi pia.

Mwandishi huyo hakutoa taarifa kwa polisi lakini alizungumzia tukio hilo katika kipindi cha mjadala mwaka wa 2007,ingawa jina la Bwana Strauss-Kahn liliondolewa.

Alidai kwamba Bwana Strauss-Kahn alimshambulia wakati alipoenda kumhoji akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili na kwamba walikabiliana vikali katika nyumba ya Strauss-Kahn,wakati alipojaribu kumfungua sidiria.

Wakili wake, David Koubbi,alisema siku ya Jumatatu kwamba mashtaka rasmi dhidi ya Bwana Strauss-Kahn yatawasilishwa siku ya Jumanne.

"Haya ni madai yenye uzito mkubwa," Bwana Koubbi alisema alipotangaza azimio la mteja wake nchini Ufaransa.

Alisema kulingana na madai hayo, tukio hilo lilifanyika mwezi wa Februari 2003,wala si 2002 kama ilivyokuwa imeripotiwa.