Ajali ya ndege yatokea DRC

Ndege ya abiria iliyokuwa na watu 112 imeanguka kwenye uwanja wa ndege wa Kisangani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Takriban watu 40 wamekutwa wakiwa hai, lakini wengine zaidi ya 50 wanasemekana kufariki dunia.

Image caption Kisangani

Ndege hiyo, iliyo chini ya shirika la ndege la Hewa Bora, ilijaribu kutua baada ya hali ya hewa kuwa mbaya ikitokea Kinshasa.

Hakuna uthibitisho bado wa aina ya ndege iliyohusishwa.

Mkurugenzi mkuu wa Hewa Bora Stavros Papaioannou aliliambia shirika la habari la Reuters, " Rubani alijaribu kutua lakini hakufanikiwa kugusa barabara ya ndege."

Msemaji wa serikali Lambert Mende alisema ndege hiyo iligonga karibu sana na uwanja wa ndege huku kukiwa na radi.

Alisema, " Tumejitahidi kuwaokoa watu 40 na harakati za uokoaji zinaendelea".

'Mbakaji' wa Congo Kanali 'Kifaru' Kulimushi ajisalimisha

Huku shughuli za uokoaji zikiendelea mwanajeshi mwenye cheo cha Kanali anayeshutumiwa kwa ubakaji wa watu wengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amejisalimisha kwa jeshi hilo.

Msemaji wa jeshi alisema Kanali Nyiragire "Kifaru" Kulimushi amejisalimisha pamoja na zaidi ya wapiganaji wake 150, wanaoshutumiwa pia kwa ubakaji wa wanawake wengi.

Haki miliki ya picha
Image caption Wanawake walioathiriwa na ubakaji

Mwezi uliopita, takriban wanawake 100 waliwashutumu waliokuwa waasi waliojiunga na jeshi la nchi hiyo kwa kuwadhalilisha kijinsia katika jimbo la Kivu ya Kusini.

Ujumbe wa umoja wa mataifa mwaka jana umeelezea nchi hiyo ya Congo kama "mji mkuu wa ubakaji duniani".

Ghasia zilizodumu miaka 16 mashariki mwa Congo zimesababisha kuenea kwa udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike.

Msemaji wa jeshi Lt Kanali Vianney Kazarama ameiambia BBC kuwa Kanali Kifaru alijisalimisha baada ya kutoka misituni kwenye ngome yake iliyopo mashariki mwa Congo.

Alisema, "walikuwa 150, na silaha zao-zikiwemo silaha nzito".