Libya: 11 wauawa Misrata

Takriban watu 11 wameuawa katika mapigano karibu na mji wa Misrata, waasi wanaokabiliana na majeshi ya Muammar Gaddafi wanasema.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Majengo yalivyoharibiwa Misrata

Waandishi wa habari mjini Misrata wanasema ngome za waasi magharibi mwa Misrata, katika eneo la Dafniya,zimeshambuliwa na wanajeshi wa Kanali Gaddafi.

Wakati huo huo,makamanda wa waasi wameiambia BBC kuwa wameunganisha wanajeshi wao wa upande wa kusini na magharibi mwa Misrata.

Waasi wanasema wanajaribu kutoka Misrata na kuelekea Tripoli sasa.

Tangu maandamano dhidi ya serikali kugeuka na kuwa vita vya kijeshi zaidi ya miezi minne iliopita,pande zote mbili zimekwama, licha ya harakati zinazoongozwa na majeshi ya angani ya Nato kusaidia waasi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waasi wanapigana na wanajeshi wa Serikali Misrata

Waasi wanadhibiti eneo la mashariki mwa Libya,pamoja na Misrata na miji mingine katika milima ya Nafusa karibu na mpaka wa Tunisia.

Mwandishi wa BBC Gabriel Gatehouse aliyeko mjini Misrata anasema mapigano ya hivi karibuni yalianza mapema siku ya Jumanne,huku milio ya risasi na mabomu yakiendelea kusikika hadi mchana.

Taarifa za mashirika ya habari zinasema kuwa ngome za waasi katika eneo la Dafniya zilishambuliwa wakati majeshi ya serikali yalipojaribu kusonga mbele.

Mfanyakazi wa hospitali moja mjini Misrata amewaambia waandishi wa shirika la habari la Reuters kuwa wapiganaji 11 wa waasi waliuawa na wengine zaidi ya kumi kujeruhiwa na mpiganaji mmoja wa waasi akawaambia waandishi wa shirika la habari la AFP kuwa watu 11 "wote wakiwa raia" wameuawa.