Al-shabaab waondoa marufuku Somalia

mkimbizi kutoka somalia Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption zaidi ya wasomali elfu moja wanaingia Kenya kila siku wakitafuta vyakula

Kundi la la Al-shabaab limetangaza kuwa litaruhusu mashirika ya kutoa misaada kusambaza vyakula nchini somalia.

Al-shabaab walipiga marufuku huduma hizo za mashirika ya kimataifa mwaka wa 2009 wakidai kuwa nia yao ilikuwa kuhujumu waislamu.

Lakini msemaji wa kundi hilo Sheikh Mohammed Ali Rage amesema wataanzisha mazungumzo na mashirika hayo kuona kuwa yanarudi kusaidia wasomali walioathirika na ukame.

Mashirika ya kutoa misaada yanasema Somalia inashuhudia kipindi kibaya zaidi cha ukame, hali iliotokea mara ya mwisho miaka 60 iliopita.

Kiongozi huyo wa Al shabaab, kundi ambalo linapinga serikali ya mpito ya Somalia amesema mashirika yote sasa ata ikiwa sio ya waislamu yanaruhusiwa kusaida raia wa nchi hiyo.

"wote sasa watakuwa huru kusaidia ili mradi tu hawatakuwa na malengo mengine" alisema Sheikh Rage.

Kundi hilo ambalo pia lina uhusiano na mtandao wa magaidi wa Al Qaeda, lilipiga marufuku mashirika hayo yakisema kuwa mengine yalikuwa yanaendesha harakati za ujasusi kwa malengo yakuliangamiza.

Katika siku za karibuni, Al shabaab wamepoteza ushawishi wao nchini Somalia na hasaa mjini Mogadishu kwenye ngome yao kufuatia makabiliano makali na wanajeshi wa serikali ya mpito wakiungwa mkono na wale wa Umoja wa Afrika.

Wadadisi wanasema uamuzi huo huenda umechochewa na hali hiyo ya kundi hilo kupoteza umaarufu wao na pia taarifa za kuwa maelfu ya raia wa somalia wanakimbilia Kenya baada ya kukabiliwa na baa la njaa.

Al-shabaab, wadadisi wanasema huenda wameaibishwa na taarifa hizo na wanajaribu kujitakasa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kutoa misaada zinaonyesha kuwa yamkini watu 1,400 wanaingia Kenya kila siku kutoka Somalia.

Wengi wao wamepewa hifadhi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab ilioko kaskazini mashariki mwa Kenya.