Waasi wasonga mbele kukaribia Tripoli

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waasi wa Libya wako kilometa 100 kusini magharibi mwa Tripoli

Waasi wa Libya wanasema wamesonga mbele katika kijiji cha Gualish kilometre 100 (maili 60) kusini magharibi mwa mji mkuu Tripoli.

Mapumziko kwenye makazi madogo jangwani ni muhimu kuelekea katika ngome kubwa mjini Garyan ambayo inadhibiti barabara kuu inayoelekea mji mkuu Tripoli.

Waasi hao walisema wamedhibiti maeneo kadhaa ya wanajeshi wa serikali.

Kwa upande wa magharibi mwa nchi vikosi vya waasi vimesonga mbele kuzunguka mji wenye bandari wa Misrata.

Taarifa zinasema waasi wanaopigana na Kanali Muammar Gaddafi walivamia Gualish siku ya Jumatano baada ya mapigano yaliyoudumu kwa saa kadhaa.

Taarifa nyingine zinasema waasi wamedhibiti maeneo muhimu ya makazi magharibi ambako kuna kituo cha Umeme na mnara wa maji.

Takriban waasi wanne wameuawa na 17 kujeruhiwa, daktari mmoja wa karibu na Yefren alisema.