Modric "kubakia Tottenham msimu huu"

Wakala wa kiungo wa Tottenham Luka Modric, Nikky Vuksan amesema mchezaji huyo hana mipango ya kupeleka barua ya kuomba uhamisho katika klabu yake.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Luka Modric

Modric anayechezea pia timu ya taifa ya Croatia, alidokeza angependa kujiunga na Chelsea, lakini Mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy ana matumaini makubwa kiungo huyo hataihama klabu yake.

Vuksan amekiambia kitengo cha michezo cha BBC: "Sidhani kama atapeleka barua ya kuomba uhamisho. Ataheshimu mkataba wake.

"Anataka kucheza ligi ya ubingwa wa Ulaya na kushinda vikombe. Njia pekee ya kutatua yote hayo ni kukaa chini na kuzungumza."

Ameongeza: "Luka ataripoti mazoezini na atajituma kama ilivyo kawaida yake."

Mapema msimu huu wa majira ya joto, Modric ilitangazwa alikuwa akiwindwa na Chelsea ambao walikuwa tayari kumnunua kwa kitita cha paundi milioni 22, fedha ambazo zilikataliwa na Spurs.

Modric alikutana na mwenyekiti wake Levy siku ya Jumatano na mwenyekiti huyo alieleza bayana kwamba mchezaji huyo hataruhusiwa kuondoka katika klabu hiyo.