Gazeti lashtumiwa kufanya udukuzi

David Cameron Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waziri Mkuu Cameron akiwa bungeni

Simu zinazomilikiwa na familia za wanajeshi wa Uingereza waliouawa inadaiwa zilifanyiwa udukuzi na gazeti la News of the World, gazeti moja la kitaifa limeandika taarifa hizo.

Gazeti la The Daily Telegraph linadai kuwa nambari za simu za jamaa za wanajeshi waliofariki dunia zilipatikana katika nyaraka za mpelelezi wa kujitegemea Glenn Mulcaire.

Haya yamejitokeza baada ya Wazir Mkuu David Cameron kusema kuwa ataunda tume kuchunguza madai hayo udukuzi wa simu.

Rupert Murdoch, anayemiliki gazeti la News of the World, ametaja madai hayo ya udukuzi kama "jambo baya sana".

Kampuni ya News International inayosimamia gazeti hilo inasema "itashangaa sana" ikiwa kutakuwa na ukweli wowote wa madai yanayohusiana na familia za wanajeshi waliofariki na kuwa itawasiliana na wizara ya Ulinzi ya Uingereza kuhusu suala hilo.

Msemaji wa kampuni hiyo amesema kuwa sifa za News International kama rafiki wa wanajeshi wa Uingereza ni nzuri sana.