Wafadhili waguswa na athari za ukame

raia wa somalia
Image caption Serikali ya uingereza tayari imetoa dola milioni 61 kusaidia walioathirika

Mashirika ya kutoa misaada nchini Uingereza yameanzisha harakati za kuchangisha pesa kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa Afrika Mashariki.

Mashirika hayo yamelenga kusaidia watu milioni 10 ambao wameathrika zaidi na ukame nchini Somalia, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini.

Tayari serikali ya Uingereza imeahidi kutoa dola milioni 61 kusaidia harakati hizo za kutoa misaada wa vyakula na huduma za matibabu katika eneo hilo.

Pesa hizo zitasaidia kutoa misaada ya dharura kwa watu milioni 1.3

Kulingana na Umoja wa Mataifa hii ndio hali mbaya zaidi ya ukame kushuhudiwa katika upembe wa Afrika kwa kipindi cha miaka 60.

Inakisiwa kuwa watu 1,300 wanahama makaazi yao nchini Somalia kila siku kuingia Kenya na Ethiopia kwa sababu ya athari za ukame.

Mashirika hayo yamebuni kamati maalumu ya kushughulikia janga hilo na yanaungwa mkono na BBC katika juhudi zao za kuchangisha pesa hizo.

Maelfu ya watu hasaa raia wa Somalia wanahitaji misaada hiyo na wengi wamepewa hifadhi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab ilioko kaskazini mashariki mwa Kenya.