Watoto 26 wafa katika ajali Bangladesh

Bangladesh
Image caption Ramani ya Bangladesh

Watoto wa shule wasiopungua 26 wamekufa baada ya Lori walimokuwa wakisafiria kutumbukia katika kijito kidogo kusini mashariki mwa Bangladesh.

Kwa mujibu wa polisi, watoto 80 walikuwa wanarejea nyumbani baada ya mashindano ya kandanda wakiwa katika lori moja lililokuwa wazi wakati lilipoteleza na kuanguka katika kijito hicho.

Ajali hiyo ilitokea katika wilaya ya Chittagong kilomita 216 kutoka mji mkuu wa Dhaka.

Maafisa wanasema idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka kwa kuwa watoto wengine inahofiwa wamenasa katika lori hilo lililozama.

Wanasema kuwa idadi ya waliokufa huenda ikawa kubwa zaidi ya iliyotajwa rasmi kutokana na kuwa bado shughuli za uwokozi zinaendelea na jamaa za watoto waliokufa huenda wamechukuwa maiti za watoto wao kabla ya hesabu rasmi kufanywa.

Awali afisa mmoja wa polisi kutoka wilaya hiyo ya Chittagong Ruhul Amin Siddiqui aliiambia BBC kuwa maiti 40 zimepatikana tayari kutoka eneo hilo la ajali.

Kwa mujibu wa walioshuhudia vijana hao walikuwa wakiimba na kucheza kabla ajali hiyo kutokea.

Ajali za barabarani nchini Bangladeshi ni tukio la kawaida ambapo watu wanaokisiwa kufika 12,000 hufa kila mwaka katika ajali mbalimbali za barabarani.Ajali nyingi hutokana na uwendeshaji mbaya wa gari, barabara mbovu na magari makuu kuu ambayo hayafai kuwa barabarani.