Arsenal yathibitisha kumsajili Gervinho

Arsenal imethibitisha kumsajili mshambuliaji hatari wa klabu ya Lille Gervinho anayechezea pia timu ya taifa ya Ivory Coast.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Gervinho

Gervinho mwenye umri wa miaka 24 ameifungia Lille mabao 15 yaliyoisaidia klabu hiyo kushinda ligi ya Ufaransa msimu uliopita.

Arsenal kwa sasa wapo katika ziara ya Mashariki ya Mbali na meneja wao Arsene Wenger amesema: "Gervinho amejiunga nasi. Alifanyiwa uchunguzi wa afya siku ya Alhamisi.

"Tumemwambia arudi nyumbani kwa siku chache kwa sababu ana familia na watoto. Hakuja nasi katika ziara kwa sababu bado hajafanya mazoezi."

Gervinho, ambaye alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast mwaka 2008 wakati wa michezo ya Olympic ya Beijing, hivi karibuni aliliambia gazeti moja la Ufaransa la michezo: "Nimeichagua Arsenal kwa sababu ni timu yenye vijana ambapo nitaweza kuzoeana nao bila matatizo."