Michael Essien kutocheza soka miezi sita

Kiungo wa klabu ya Chelsea Michael Essien hatacheza soka kwa muda wa miezi sita baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.

Image caption Michael Essien

Essien ambaye pia huchezea timu ya taifa ya Ghana aliumia goti wakati akifanya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya na upasuaji wa goti lake imeelezwa "ulikwenda" vizuri.

Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas ameeleza katika mtandao wa klabu hiyo: "Kila mmoja anamtakia Michael apone haraka.

"Wachezaji wenzake na wafanyakazi wote pamoja na mimi tupo tayari kumsaidia aweze kurejea uwanjani haraka iwezekanavyo."

Mwaka 2008 Essien hakucheza soka kwa muda wa zaidi ya miezi sita baada ya kuumia goti.

Pia hakuweza kuiwakilisha Ghana katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 kwa sababu ya matatizo hayo hayo ya goti.