Mzimbabwe ashinda tuzo ya Caine

Haki miliki ya picha other
Image caption NoViolet Bulawayo kutoka Zimbabwe

Mwandishi kutoka Zimbabwe NoViolet Bulawayo ameshinda tuzo ya Caine inayotolewa kwa waandishi wa Afrika, inayochukuliwa kama tuzo inayoongoza ya Afrika kwenye uandishi.

Amepata zawadi hiyo ya dola za kimarekani 10,000 baada ya kuandika hadithi iitwayo 'Hitting Budapest' kuhusu watoto wenye njaa mtaa wa mabanda wanaoiba mapera kutoka kwenye kitongoji kimoja.

Aliiambia BBC: " Hujaribu kuandika habari ambazo si aghlabu kusimuliwa."

"Lugha iliyotumika kwenye hadithi hiyo ya Hitting Budapest ni bora," alisema mkuu wa jopo la majaji Hisham Matar, aliyemtangaza mshindi kwenye sherehe za kutoa tuzo hiyo mjini Oxford, Uingereza Jumatatu jioni.

"Hii ni hadithi yenye uadilifu na uzito. NoViolet Bulawayo ni mwandishi anayefurahia kutumia lugha."

Mwanzo wa hadithi hiyo, iliyochapishwa mwaka jana, mtangazaji anaelezea kwanini watoto wanaelekea Budapest: "kuna mapera ya kuiba Budapest, na kwa sasa nitakufa kwa ajili ya mapera, au lolote kwa maana hiyo."

Bi Bulawayo aliiambia BBC, " Huko hukabiliana na mwanamke kutoka London ambaye ana nia zaidi ya kuwapiga picha, ambalo nadhani hufanywa sana na watu kutoka nchi za magharibi wanapokwenda Afrika, lakini anashindwa kutambua kuwa wana njaa."

Mmoja wa watoto hao ni binti mwenye umri wa miaka 10 aliyetiwa ujauzito na babu yake.

Alisema, "si sahihi asilan, lakini kwenye mazingira haya ni jambo la kawaida."

Bi Bulawayo alisema anajiona kama ni yeye katika hadithi hiyo.

"Baadhi ya matukio katika Hitting Budapest yametokana na maisha yangu halisi- kwa kuanzia pale ninapohadithia kuiba mapera, kukua nikiwa sina fursa nyingi na kuwa na ndoto za baadae."

NoViolet Bulawayo alizaliwa na kulelewa Zimbabwe na hivi karibuni amefanikiwa kukamilisha shahada ya uzamili katika chuo kikuu cha Cornell nchini Marekani.