'Mapigano makali' mji wa mafuta Libya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waasi Libya

Waasi wa Libya wamesema wanapigana na majeshi ya Muammar Gaddafi katika maeneo ya makazi ya watu mjini Brega mashariki mwa nchi hiyo.

Majeshi ya waasi yamekuwa yakisogea Brega kwa siku kadhaa sasa licha ya makombora mazito kurushwa na majeshi ya serikali yaliyodhibiti mji huo.

Haijawezekana kuthibitisha madai hayo ya waasi.

Waandishi walisema, kuporomoka kwa mji huo, kituo cha moja ya viwanda vikubwa sana vya mafuta nchini Libya, itakuwa mafanikio makubwa kwa majeshi yanayompinga Kanali Gaddafi.

Brega, takriban kilomita 750 mashariki mwa mji mkuu Tripoli, imejikuta kwenye mapigano mara nyingi tangu ghasia kuanza mwezi Februari.

Mohammed Zawi, msemaji wa majeshi ya waasi, alinukukuliwa na shirika la habari la AFP akisema, "Baadhi ya vikundi vidogo vimefanikiwa kuingia, lakini bado hatujadhibiti mji wote."

Alisema, "Kwa sasa tunapigana kwa karibu sana."

Katika hatua nyingine tofauti siku ya Jumatatu, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, aliyeongoza ujumbe wa upatanishi kwa niaba ya Umoja wa Afrika, alisema Libya inahitaji serikali ya kidemokrasia.

Lakini alisema watu wa Libya lazima waamue hatima yao wenyewe, na iwapo Kanali Gaddafi ataondoka lazima kuwe na masharti ya lini, wapi na ni namna gani hatua hiyo itafanyika.

Wakati huo huo, Urusi imekataa kutambua uongozi wa waasi kama serikali halali ya Libya.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema hatua hiyo itasababisha mgawanyiko katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Marekani na mataifa mengine ya kimagharibi na kiarabu yalipotambua upinzani wa Libya kuwa "serikali halali" na kurudia matakwa yao kwamba Kanali Gaddafi na familia yake waachie madaraka.