UN yaonya kuhusu uhalifu Sudan

Ripoti ya umoja wa mataifa imeonya kuwa uhalifu wa kivita huenda ukawa umefanywa katika mji wa Kordofan Kusini nchini Sudan

Ripoti hiyo, iliyofichuliwa na BBC, ilisema serikali na majeshi ya waasi yote yana hatia ya kufanya ukatili japo yaliyofanywa na jeshi la serikali "ni ya kushtusha zaidi".

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Picha ya makaburi Kordofan Kusini

Imetoa wito wa kufanywa uchunguzi maalum katika mgogoro huo, uliosababisha watu takriban 70,000 kuhama makazi yao.

Serikali ya Sudan ilisema inajibu mashambulio dhidi ya waasi kwenye mji unaopakana na Sudan Kusini.

Mwandishi wa BBC James Copnall kwenye mji mkuu, Khartoum, amesema ripoti hiyo inaelezea kuhusu mauaji ya kinyama na mashambulio ya anga.

Mmoja aliyeshuhudia amewaambia wachunguzi wa umoja wa mataifa kuwa aliona miili 150 kwenye ngome ya kijeshi Kordofan kusini.

Ripoti hiyo imesema baraza la usalama la umoja wa mataifa liunde tume itakayochunguza madai, bila shaka kwa usaidizi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita.

Iwapo madai haya ni ya kweli, basi yatatajwa kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, ripoti hiyo imesema.