Murdoch atakiwa ajieleze kwa Wabunge

Tajiri anayemiliki magazeti mengi hapa Uingereza, Marekani na Australia chini ya kampuni ya News Corporation, Rupert pamoja na mwanae James Murdoch wametakiwa wafike mbele ya wabunge wa Uingereza wajibu masuali kuhusiana na kashfa ya udukuzi wa simu za watu siku ya jumanne.

Image caption Rupert Murdoch

Lakini kama raia wa Marekani, Rupert Murdoch, amepinga ombi la kufika na kujibu masuali ya wabunge wa Kamati inayohusika na vyombo vya habari, na mwanae James aliyejitolea kwenda siku aitakae yeye, hawezi kushurutishwa.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni yao Rebekah Brooks amekubali kufika na kuhojiwa.

Wakati hayo yakiendelea mwanamme mwenye umri wa miaka 60, ametiwa mbaroni kuhusiana na udukuzi wa simu.

BBC imefahamu kuwa mtu huyo ni Neil Wallis,hapo zamani Mhariri mkuu wa gazeti la News of the World. Bw Wallis alikamatwa na Maofisa kutoka idara maalum ijulikanayo kama Operating Weeting mapema Alahamisi na kupelekwa kwenye kituo cha polisi London ya magharibi kwa tuhuma za kuingilia mawasiliano.

Neil Wallis, hapo zamani alikuwa mwanachama wa Kamati ya wahariri inayohimiza maadili katika uandishi wa habari, ni mtu wa tisa kukamatwa tangu Polisi wa London waanze upelelezi mpya katika kashfa ya udukuzi mnamo mwezi januari.

Gazeti la News of the World linalomilikiwa na familia ya Murdoch lilifunga shughuli zake wiki iliyopita kufuatia kashfa hiyo ya kudukuza simu za watu waliofikwa na misiba, wanasiasa pamoja na watu maarufu.

Masuala nyeti Siku ya Jumanne, Kamati ya bunge inayohusika na utamaduni, vyombo vya habari na michezo ilimtaka Bi.Brooks pamoja na familia ya Murdoch ijitokeze kuhusu madai ya udukuzi wa simu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bi Brooks na Murdoch

Katika taarifa, wabunge walisema kuwa kuna masuali nyeti kuhusu ushahidi muhimu uliotolewa na Bi.Brooks pamoja na Andy Coulson, wote ambao zamani walikuwa wahariri wa News of the World walipohojiwa mwaka 2003.

Katika barua yake kwa Mwenyekiti wa kamati hiyo John Whittingdale, Bw.Rupert Murdoch alisema kuwa ingawa hatoweza kujitokeza siku ya jumanne kama walivyomtaka afanye, yuko tayari kutoa ushahidi kamili, kutoa ushahidi kwa Tume inayoongozwa na Jaji iliyotangazwa na Waziri mkuu David Cameron.

Mtoto wa tajiri huyo, James Murdoch alijitolea kua angeweza kufika mbele ya Kamati siku nyingine, labda tareh 10 agosti.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption James na Rupert Murdoch

Lakini katika taarifa yao, Wabunge wamesema kuwa: Kamati ya bunge inabainisha kuwa imetambua kuwa itakuwa muhimu kwa wahusika wote wajitokeze kuelezea tabia na sababu za kampuni ya News International na vilevile kuhusiana na maelezo yaliyotolewa mbele ya Kamati ya bunge, kwa sasa maelezo ambayo, tunakiri hayakuwa na ukweli.

Halikadhalika, Kamati hiyo imeamua kumuita Rupert Murdoch na James Murdoch wafike mbele ya Kamati hiyo maalum, saa nane unusu Jumanne tareh 19 julai mwaka 2011.

Bw.Whittingdale amesema kuwa Naibu msimamizi wa mahakama bungeni yeye binafsi ndiye atakayewasilisha waraka wa kuwataka akina Murdoch wafike mbele ya Kamati.