Kaburi la pamoja lagunduliwa Sudan

Makaburi  ya wengi Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Makaburi ya wengi

Picha za Satellite zimeonyesha makaburi ya watu wengi waliozikwa pamoja kutokana na mapigano ya hivi karibuni nchini Sudan. Hayo ni kwa mujibu wa kikundi cha kutetea haki za binaadamu kilichoundwa na mcheza senema wa Hollywood George Clooney.

Kikundi hicho kiitwacho Satellite Sentinel kinasema kile kinachodhaniwa ni kuwa mauaji yamefanyika katika mji wa Kadugli,Kordofan kusini.

Mapigano yalianza katika jimbo hilo mnamo mwezi uliopita ,kati ya waasi kutoka milima ya Nuba na vikosi vya kijeshi vya Sudan.

Msemaji wa kijeshi wa Sudan amekanusha madai kuwa raia waliuawa.

Kordofan Kusini inapakana na Sudan Kusini ambayo mnamo wiki iliyopita ilikua taifa huru.

Kikundi hicho cha "The Satellite Sentinel project " kinasema picha za satellite zinaambatana na madai kuwa majeshi ya Sudan na wanamgambo washirika wa serikali wamekuwa wakiwalenga raia.

Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa ilisema mashambulio ya mabomu na mapigano yaliendelea Kordofan Kusini licha ya kutiwa saini mapatano ya amani.

Mwandishi wa BBC James Copnall akiwa mji mkuu wa Sudan Khartoum anaarifu kwamba ni vigumu sana kupata taarifa za uhakika kwa kuwa waandishi habari na wanabalozi wamepigwa marufuku katika eneo hilo na shughuli za Umoja wa Mataifa zimeekewa vikwazo.

Kikundi hicho pia kinasema kimezungumza na mashahidi kadhaa wanaodai kuwa wapiganaji wanaoshikamana na serikali ya Sudan yanaendesha kampeni ya mauaji ya mfululizo dhidi ya raia wanaoaminiwa kuwa wanaipinga serikali.

Rais Barack Obama amekwishaelezea wasiwasi wake kuhusu mashambulio katika Kordofan kusini kwa misingi ya kikabila. Khartoum inakanusha madai hayo na kusema inapigana vita halali vya kujilinda dhidi ya waasi.

Wakaazi wengi wa milima ya Nuba walipigana bega kwa bega na waasi wa Sudan kusini katika vita vya zaidi ya miaka 20 kati ya kusini na kaskazini lakini sasa wanajikuta wakiwa upande wa kaskazini.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema atashirikiana na Rais Omar al Bashir wa Sudan kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa.