FBI yachunguza kampuni ya Murdoch

Idara ya upelelezi nchini marekani FBI, imeanzisha uchunguzi kubaini ikiwa shirika la News Corporation lilihusika na udakuzi wa simu za walioathirika na shambulio la Septemba 11, mjini New York.

Haki miliki ya picha AP
Image caption sakata hiyo imekwamisha mipango ya Murdoch kununua BskyB

Upelelezi huo umeanzishwa kufuatia shinikizo kutoka baadhi ya wajumbe wa baraza la senate na vigogo wa chama cha Republican.

Hata hivyo, mmiliki wa shirika hilo la vyombo vya habari, Rupert Murdoch ametetea kampuni yake akisema suala hilo lilishughulikiwa kwa njia inayofaa.

Murdoch na mtoto wake James, wamekubali kufika mbele ya kamati ya mawasiliano ya bunge la Uingereza kujibu maswali kuhusu sakata hiyo ya udakuzi.

Awali mwekezaji huyo maarufu alipuuza agizo hilo la kamati ya bunge.

Nchini Marekani, duru za kuaminika kutoka FBI zimefuchua kuwa uchunguzi unaendelea dhidi ya waandishi wa gazeti News of The World.

Waandishi hao inadaiwa walifanyia udakuzi simu za jamaa za walioathirika na shambulio la Septemba 11 miaka kumi iliopita.

Mapema wiki hii, masenta wa chama tawala cha Democratic walimshauri mkuu wa sheria achunguze ikiwa shirika hilo la habari lilikiuka sheria za marekani kwa kusikiliza mawasiliano hayo ya simu.

Kasheshe hiyo inayokabili shirika la News Corporation lenye makao makuu nchi Marekani, imehujumu mpango wake wa kununua kampuni kubwa zaidi ya huduma za televeshini za kulipia nchini Uingereza BskyB.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, ameteua tume maalum inayoongozwa na jaji kuchunguza sakata hiyo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa dhidi ya wahusika.